Taasisi isiyo ya kiserikali ya Pink Hijab ambayo inajihusisha na kuwahamasisha kimaendeleo wanawake na vijana katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ikiwemo kuwapa elimu ya kimaisha imeandaa maonesho makubwa ya bidhaa za kiujasiriamali za kinamama na vijana.
Akizungumza na Wanahabari, Afisa Uhusiano na Jinsia wa Pink Hijab, Zabihuna Omari, amesema maonesho hayo yanatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Utamaduni wa Watu wa Irani jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 4 mpaka 6 mwaka huu ambapo kinamama hao watakuwa wakiuza na kuonesha uzalishaji wa bidhaa zao mbalimbali.
Zabihuna amesema katika maonesho hayo, Pink Hijab itazindua mpango wake unaoitwa Hadija Initiative ambao lengo lake kuu ni kuwaongezea nguvu kinamama na vijana kwenye masuala mazima ya kibiashara.
Amesema katika kuwaongezea nguvu kina mama hao ni pamoja na kuwaunganisha na kinamama wengine waliobobea katika Nyanja za kibiashara kutoka mataifa mbalimbali.
Naye mwakilishi wa wafanyabiashara wa Pink Hijab App, Francisca Lymo amesema wao watashiriki katika maonesho hayo ambayo yameanzishwa na Pink Hijab kwa ajili ya kuwahamasisha wanawake kujiona kuwa wanaweza kufanya chochote wanachohitaji bila kutegemea nguvu ya mtu mwingine.
Ameendelea kusema;
“Simama jiwezeshe, hiyo ndiyo kauli yetu ya sasa na siyo ile kauli iliyopitwa na wakati ya mwanamke akiwezeshwa anaweza kwanini uwezeshwe sasa hivi wenyewe tunaweza Pink Hijab inafanya wanawake tujiwezeshe” alimaliza kusema Francisca.
Yuse Hozza ambaye ni mwanachama wa Pink Hijab kwa upande wake amewakaribisha wote kwenye maonesho hayo na kuwasisitiza wababa wenzake wasikose kwenye maonesho hayo na kusema katika mafanikio ya kinamama ni sehemu ya mafanikio ya kinababa.
Mariam Yusuf ambaye ni mwanzilishi wa taasisi ya Girl and Graphics ambayo inahusika na kuwafundisha mabinti elimu ya Graphics naye amewakaribisha mabinti wenzake kufika kwenye maonesho hayo na kuweza kujifunza masuala ya Graphic na mengineyo ya kiujasiriamali. HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS /GPL